El Clasico, klabu nguli za Hispania Real Madrid na Barcelona zitakapokwaana, ni miongoni mwa mechi kubwa zinazosubiriwa kwa hamu sana kwenye ulimwengu wa soka.
Kule Hispania ni zaidi ya mechi ya soka; ni mtanange wa kiutamaduni, uliogubikwa na itikadi, kadhalika kuonyeshana umwamba baina ya wachezaji wawili bora duniani.
Cristiano Ronaldo dhidi ya Lionel Messi ndilo tukio kuu dunia itakapogeuzia macho pambano hilo, kuamua kwa mara ya tisa, nani mbabe katika mechi hiyo ya miungu wa soka.
Mahasimu hao wanapojiandaa kwa mechi hiyo kubwa, Goal inakuangazia takwimu kuona nani yupo juu ya mwenzake kwenye Clasico.
NANI AMESHINDA MECHI NYINGI ZA CLASICO?
Messi ameshinda mechi ngapi za Clasico?
Mechi | Ameshinda | Sare | Amepoteza |
---|---|---|---|
36 | 16 | 8 | 12 |
Inapokuja kwenye mafanikio ya Clasico, Messi amekuwa upande unaoshinda mara nyingi zaidi ya Ronaldo, akishinda mechi 16 dhidi ya Real Madrid kwenye michuano yote.
Mwargentina huyo amecheza dhidi ya mahasimu wakubwa wa Barca mara 36 kipindi chake cha soka katika michuano tofauti tofauti. Katika mechi hizo 36, Messi ameonja vipigo 12 na kutoa sare nane.
La Liga ndio uwanja wa raha kwenye mafanikio ya Clasico, ushindi 12 kati ya 16 ukipatikana kwenye michuano hiyo.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, Messi hajawahi kupoteza mechi kwa Real Madrid, wakiwa wamepata sare na ushindi katika mechi mbili alizoshiriki.
Cristiano Ronaldo ameshinda Clasico ngapi?
Mechi | Ameshinda | Sare | Amepoteza |
---|---|---|---|
28 | 8 | 6 | 13 |
Mafanikio ya Ronaldo kwenye mechi za Clasico yapo chini ukilinganisha na yale ya Messi, lakini ni lazima ifahamike kuwa Mreno huyo amecheza mechi chache, baada ya kujiunga na Real mwaka 2009 - misimu kadhaa baada ya Messi kuanza kuichezea Barca.
Ronaldo amekuwa upande wa ushindi katika mechi nane tu kati ya Clasico 28, akipoteza 13 na kupata sare sita.
NANI AMEFUNGA MAGOLI MENGI KWENYE CLASICO?
Messi amefunga magoli mangapi Clasico?
Mechi | Magoli | Mashuti | Mashuti yaliyokuwa goli |
---|---|---|---|
36 | 24 | 125 | 19.72% |
Kwa mara nyingine, Messi amekuwa juu kwa mabao aliyofunga kwenye Clasico, akitikisa nyavu mara 24 kwenye mechi 36 baina ya timu hizo.
Magoli mengi yamepatikana La Liga, akiweka kimiani mara 16 katika mechi 22, sita yakipatikana kwenye mechi sita za Supercopa na mawili kwenye Ligi ya Mabingwa.
Michuano pekee ambayo Messi hajafunga dhidi ya Real Madrid ni Copa del Rey baada ya kunyamazishwa kwenye mechi sita.
Magoli mangapi ya Clasico amefunga Ronaldo?
Mechi | Magoli | Mashuti | Mashuti yaliyokuwa goli |
---|---|---|---|
28 | 17 | 117 | 22.5% |
Ronaldo yupo nyuma ya Messi kwa magoli saba kwenye mechi za Clasico akiwa na mabao 17, lakini tofauti hiyo haina maana sana kwani mshindi huyo wa Ballon d'Or amecheza mechi nane pungufu ya hasimu wake.
Uwiano wa Messi wa magoli na mechi ni bora kidogo kuliko wa Ronaldo (0.66 hadi 0.6), ingawa mpinzani wake wa Kireno amejaribu kupiga mashuti mengi zaidi kwa mchezo.
NANI MWENYE PASI NYINGI ZA GOLI?
Messi ametoa pasi ngapi za goli?
Mechi | Pasi za goli | Nafasi alizotengeneza |
---|---|---|
36 | 13 | 65 |
Ronaldo ametoa pasi ngapi za goli kwenye Clasico?
Mechi | Pasi za goli | Nafasi alizotengeneza |
---|---|---|
28 | 1 | 14 |
RONALDO VS MESSI: CLASICO KWA UJUMLA
Mchezaji | Clasico walizoshinda | Magoli | Pasi za goli |
---|---|---|---|
Lionel Messi | 16 | 24 | 13 |
Cristiano Ronaldo | 8 | 17 | 1 |
Amekuwa wa pili nyuma ya Ronaldo kwa mataji na tuzo binafsi mwaka jana, lakini Messi bado ni mfalme wa Clasico.
Mwargentina huyo amefunga magoli mengi zaidi, na kutoa pasi nyingi zaidi za goli na amekuwa upande unaoshinda zaidi Barca inapoikabili Real.
Messi ana uwiano mzuri wa magoli kwa mechi na takwimu zinaonyesha wazi kwamba mchango wake ni mkubwa kwa timu yake Barca kuliko anavyofanya Ronaldo kwa Madrid.
No comments:
Post a Comment