KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amekuwa msaada mkubwa kwa mshambuliaji Heritier Makambo ambaye kwa sasa anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 11 kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Ajibu ambaye mpaka sasa ana asisti 13 msimu huu, amehusika katika mabao manne kati ya 11 yaliyofungwa na Makambo.
Katika jumla ya mabao 35 ambayo Yanga imeyafunga mpaka sasa kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi 50 kileleni, Ajibu ameonekana kumtengenezea Makambo nafasi nyingi za kufunga kuliko mchezaji yeyote kikosini hapo.
Asisti ambazo Ajibu amempatia Makambo mpaka sasa ni katika mchezo dhidi ya Coastal Union ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Pia katika mchezo dhidi ya Alliance ambao nao ulichezwa Uwanja wa Taifa, Yanga walishinda mabao 3-0, Ajibu alimpa asisti moja Makambo. Mechi dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Yanga walishinda 3-2 na Ajibu alimpa Makambo asisti moja, huku asisti ya nne ya Ajibu kwa Makambo ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City ambapo Yanga ilishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
No comments:
Post a Comment