KOCHA mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems amesema katika mechi zao 24 za Ligi Kuu Bara zilizobaki, hawatafungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa lengo la kuipiku Yanga na kutetea ubingwa wao.
Mbelgiji huyo alisema kuwa licha ya wapinzani wao Yanga kuwa juu katika msimamo wa ligi hiyo siyo kigezo cha wao kushindwa kutetea ubingwa wao.
Yanga inaongoza msimamo wa ligi kuu kwa pointi 50 baada ya mechi 18 huku Simba ikiwa na alama 33 katika michezo 14 ikiwa na viporo vinne.
Katika mechi 24 ambazo Simba imesalia kuzicheza msimu huu imesaliwa na mechi takribani 13 dhidi ya Azam (2), Yanga, Mbao, Mtibwa Sugar, Coastal Union, KMC, Kagera Sugar, JKT Tanzania, Ndanda, Mwadui FC, Ruvu Shooting, Biashara United mechi hizo zote zitachezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha huyo alisema kuwa mahesabu ya kushinda mechi za nyumbani ni muhimu ili kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2018/19.
“Sina hofu na spidi ya Yanga katika ligi na Azam hawanitishi sababu mpango wangu baada ya mechi ya Singida ni kushinda mechi zote ambazo tutakuwa katika uwanja wa nyumbani mpaka msimu unamalizika katika mechi 24 zilizosalia.
“Timu yangu itakaposhinda mechi zote za nyumbani ni wazi nafasi ya kutetea ubingwa kwetu iko palepale na ni lazima kupambana kwa hilo sababu ndiyo nafasi pekee ambayo tumesalia nayo ili msimu ujao tushiriki tena michuano ya kimataifa kama ilivyo sasa,” alisema Mbelgiji huyo.
No comments:
Post a Comment